‏ 1 Chronicles 18

Ushindi Wa Daudi

(2 Samweli 8:1-18)

1Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akautwaa Gathi pamoja na vijiji vinavyouzunguka kutoka utawala wa Wafilisti.

2 aPia Daudi akawashinda Wamoabu, wakawa watumishi wake, nao wakawa wanamletea ushuru.

3 bZaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mfalme wa Soba, hadi Hamathi, wakati alikwenda kuimarisha utawala wake katika Mto Frati. 4 cDaudi akateka magari ya vita 1,000 miongoni mwa magari yake, waendesha hayo magari ya kukokotwa na farasi 7,000 na askari wa miguu 20,000. Daudi akakata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wakokotao magari, ila akabakiza 100.

5 dWaaramu wa Dameski, walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao. 6 eDaudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski. Basi Waaramu wakawa watumwa wa Daudi, na kumlipa ushuru. Bwana akampa Daudi ushindi kote alipokwenda.

7Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu. 8 fKutoka miji ya Tibhathi na Kuni, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi sana, ambayo Solomoni aliitumia kutengenezea ile Bahari ya shaba, zile nguzo na vifaa mbalimbali vya shaba.

9Tou mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, 10 gakamtuma mwanawe, Hadoramu kwa Mfalme Daudi ili kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Mfalme Hadadezeri, kwa kuwa alikuwa amepigana vita mara nyingi na Tou. Hadoramu akamletea Daudi vifaa mbalimbali vya dhahabu, fedha na shaba.

11 hMfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Bwana kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu aliyokuwa ameitwaa katika mataifa yote haya: Edomu na Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki.

12 iAbishai mwana wa Seruya akawaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi. 13 jAkaweka kambi za askari walinzi huko Edomu, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. Bwana akampa Daudi ushindi kila alipokwenda.

Maafisa Wa Daudi

14 kDaudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote. 15 lYoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu; 16 mSadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Shausha alikuwa mwandishi; 17 nnaye Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa maafisa wakuu katika utumishi wa mfalme.

Copyright information for SwhNEN