1 Kings 3:1-15
Solomoni Anaomba Hekima
(2 Nyakati 1:3-12)
1 aSolomoni akafanya urafiki na Mfalme Farao wa Misri na kumwoa binti yake. Akamleta huyo binti katika Mji wa Daudi mpaka alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la Bwana, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu. 2Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye vilima, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la Bwana. 3 bSolomoni akaonyesha upendo wake kwa Bwana kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu.4 cMfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia, naye Solomoni akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu. 5 dBwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”
6Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.
7 e“Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. 8 fMtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. 9 gHivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”
10 hBwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili. 11 iBasi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, 12 jnitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako. 13 kZaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. 14Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.” 15Ndipo Solomoni akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto.
Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.
Copyright information for
SwhNEN