2 Kings 25:1-21
Kuanguka Kwa Yerusalemu
(2 Nyakati 36:13-21; Yeremia 52:3-30)
1 aHivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote. 2Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia. 3 bIlipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu. 4 cKisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. 5 dLakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia mfalme na kumpata katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, 6 enaye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, mahali ambapo hukumu yake ilitangazwa. 7 fWakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayangʼoa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.8Mnamo siku ya saba ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme, afisa wa mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu. 9 gAlichoma moto Hekalu la Bwana, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu. 10 hJeshi lote la Wakaldayo, chini ya jemadari wa askari walinzi wa mfalme, walivunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu. 11 iNebuzaradani jemadari wa askari walinzi akawapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli. 12 jLakini yule jemadari wa askari walinzi akawaacha baadhi ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
13Wakaldayo walivunja vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Bwana. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli. 14 kWakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu. 15 lJemadari wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.
16Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana, ilikuwa na uzito usioweza kupimika. 17 mKila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane. ▼
▼Dhiraa 18 ni sawa na mita 8.2.
Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu ▼▼Dhiraa 3 ni sawa na mita 1.35.
na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza. 18 pYule jemadari wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu. 19Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji. 20Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. 21 qHuko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe.
Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.
Copyright information for
SwhNEN