‏ 2 Samuel 9

Daudi Na Mefiboshethi

1 aDaudi akauliza, “Je, hakuna mtu hata mmoja wa nyumba ya Sauli aliyebaki ambaye naweza kumtendea wema kwa ajili ya Yonathani?”

2 bBasi palikuwepo mtumishi wa nyumba ya Sauli aliyeitwa Siba. Wakamwita aje mbele ya Daudi, naye mfalme akamwambia, “Wewe ndiwe Siba?”

Akamjibu, “Naam, mimi ndiye mtumishi wako.”

3 cMfalme akauliza, “Je, hakuna yeyote ambaye amebaki wa nyumba ya Sauli ninayeweza kumwonyesha wema wa Mungu?”

Siba akamjibu mfalme, “Bado yupo mwana wa Yonathani, yeye ni kiwete miguu yote.”

4 dMfalme akauliza, “Yuko wapi?”

Siba akajibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-Debari.”

5Basi Mfalme Daudi akamtaka aletwe kutoka Lo-Debari, kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli.

6 eMefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, alipofika kwa Daudi, akainama kumpa mfalme heshima.

Daudi akamwita, “Mefiboshethi!”

Mefiboshethi akajibu, “Ndimi mtumishi wako.”

7 fDaudi akamwambia, “Usiogope, kwa maana hakika nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Nitakurudishia ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli baba yako, nawe daima utakula chakula mezani pangu.”

8 gMefiboshethi akasujudu akasema, “Mimi mtumishi wako ni nini hata uangalie mbwa mfu kama mimi?”

9 hNdipo mfalme akamwita Siba mtumishi wa Sauli na kumwambia, “Nimempa mwana wa bwana wako kila kitu kilichokuwa mali ya Sauli na jamaa yake. 10 iWewe, wanao na watumishi wako mtamlimia mashamba Mefiboshethi na kumletea mavuno, ili kwamba mwana wa bwana wako apate mahitaji yake. Naye Mefiboshethi mwana wa bwana wako atakula chakula mezani pangu daima.” (Siba alikuwa na wana kumi na watano, na watumishi ishirini.)

11 jNdipo Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya chochote bwana wangu mfalme atakachoagiza mtumishi wake kufanya.” Basi Mefiboshethi akala chakula mezani pa Daudi kama mmoja wa wana wa mfalme.

12 kMefiboshethi alikuwa na mwanawe mdogo aliyeitwa Mika, nao watu wote wa nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi. 13 lNaye Mefiboshethi akaishi huko Yerusalemu, kwa sababu daima alikula mezani pa mfalme, naye alikuwa kiwete miguu yote.

Copyright information for SwhNEN