‏ Esther 5

Ombi La Esta Kwa Mfalme

1 aSiku ya tatu, Esta alivaa mavazi yake ya kimalkia, naye akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, mbele ya ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa akiketi katika kiti chake cha kifalme katika ukumbi, akielekea langoni. 2Alipomwona Malkia Esta amesimama uani alipendezwa naye, akamnyooshea fimbo ya utawala ya dhahabu ile iliyokuwa mkononi mwake. Kwa hiyo Esta alikaribia na kuigusa ncha ya fimbo ya mfalme.

3 bKisha mfalme aliuliza, “Malkia Esta, ni nini? Ombi lako ni nini? Hata kama ni nusu ya ufalme, utapewa.”

4Esta akajibu, “Kama itampendeza mfalme, mfalme pamoja na Hamani waje leo katika karamu ambayo nimeiandaa kwa ajili yake.”

5Mfalme akasema, “Mleteni Hamani mara moja, ili tupate kufanya lile Esta analoomba.”

Kwa hiyo mfalme na Hamani walihudhuria karamu aliyoiandaa Esta.
6 cWalipokuwa wakinywa mvinyo mfalme akamuuliza Esta tena, “Sasa haja yako ni nini? Utapewa. Ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme, utapewa.”

7Esta akajibu, “Haja yangu na ombi langu ni hili: 8 dKama mfalme ameona vyema, nami nimepata kibali kwake na kama ikimpendeza mfalme kunipa ombi langu na kunitimizia haja yangu, mfalme na Hamani waje kwangu kesho katika karamu nitakayowaandalia. Kisha nitajibu swali la mfalme.”

Ghadhabu Ya Hamani Dhidi Ya Mordekai

9 eHamani alitoka siku hiyo kwa furaha na moyo mchangamfu. Lakini alipomwona Mordekai langoni mwa mfalme na kuona kwamba hakusimama wala hakuonyesha hofu mbele yake, alijawa na ghadhabu dhidi ya Mordekai. 10 fHata hivyo, Hamani alijizuia akaenda zake nyumbani.

Akawaita pamoja rafiki zake na Zereshi, mkewe.
11 gHamani akajisifia kwao juu ya utajiri wake mwingi, wanawe wengi na kwa njia zote ambazo mfalme amemheshimu kwazo na jinsi alivyomweka juu ya wakuu na maafisa wengine. 12Hamani akaongeza, “Si hayo tu. Mimi ndiye mtu pekee ambaye Malkia Esta amemwalika kumsindikiza mfalme kwenye karamu aliyomwandalia. Naye amenialika pamoja na mfalme kesho. 13Lakini haya yote hayanipi kuridhika iwapo ninaendelea kumwona yule Myahudi Mordekai akiketi kwenye lango la mfalme.”

14 hZereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, “Tengeneza mahali pa kuangika watu kimo chake dhiraa hamsini,
Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5.
kisha kesho asubuhi mwombe mfalme Mordekai aangikwe juu yake. Ndipo uende na mfalme kwenye karamu kwa furaha.” Shauri hili lilimpendeza Hamani, naye akajenga mahali pa kuangika watu.

Copyright information for SwhNEN