‏ Job 3

Sehemu Ya Pili: Mazungumzo Ya Ayubu Na Rafiki Zake Watatu

(Ayubu 3–31)

Hotuba Ya Kwanza Ya Ayubu

Ayubu Anazungumza

1 aBaada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.

2Kisha akasema:

3 b“Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali,
nao usiku ule iliposemekana,
‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’
4Siku ile na iwe giza;
Mungu juu na asiiangalie;
nayo nuru isiiangazie.
5 cGiza na kivuli kikuu kiikalie tena;
wingu na likae juu yake;
weusi na uifunike nuru yake.
6 dUsiku ule na ushikwe na giza kuu;
usihesabiwe katika siku za mwaka,
wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote.
7 eUsiku ule na uwe tasa;
sauti ya furaha na isisikike ndani yake.
8 fWale wazilaanio siku wailaani hiyo siku,
wale walio tayari kumwamsha Lewiathani.
Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa.

9 hNyota zake za alfajiri na ziwe giza;
nao ungojee mwanga bila mafanikio,
wala usiuone mwonzi wa kwanza
wa mapambazuko,
10kwa sababu huo usiku haukunifungia
mlango wa tumbo la mama yangu,
ili kuyaficha macho yangu
kutokana na taabu.

11 i“Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa?
Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?
12 jKwa nini pakawa na magoti ya kunipokea
na matiti ili nipate kunyonyeshwa?
13 kKwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani.
Ningekuwa nimelala na kupumzika
14 lpamoja na wafalme na washauri wa dunia,
waliojijengea mahali ambapo sasa ni magofu,
15 mpamoja na watawala waliokuwa na dhahabu,
waliozijaza nyumba zao kwa fedha.
16 nAu kwa nini sikufichwa ardhini kama mtoto aliyezaliwa mfu,
kama mtoto mchanga ambaye kamwe hakuuona mwanga?
17 oHuko waovu huacha kusumbua
na huko waliochoka hupumzika.
18 pWafungwa nao hufurahia utulivu wao,
hawasikii tena sauti ya kukemea ya kiongozi wa watumwa.
19 qWadogo na wakubwa wamo humo,
na mtumwa ameachiwa huru kutoka kwa bwana wake.

20 r“Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni,
na hao wenye uchungu kupewa uhai,
21 swale wanaotamani kifo ambacho hakiji,
wale watafutao kufa zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,
22 tambao hujawa na furaha,
na hushangilia wafikapo kaburini?
23 uKwa nini uhai hupewa mtu
ambaye njia yake imefichika,
ambaye Mungu amemzungushia boma?
24 vKwa maana kulia kwangu kwa uchungu kwanijia badala ya chakula;
kusononeka kwangu kunamwagika kama maji.
25 wLile nililokuwa naliogopa limenijia;
lile nililokuwa ninalihofia limenipata.
26 xSina amani, wala utulivu;
sina pumziko, bali taabu tu.”
Copyright information for SwhNEN