Mark 1
Mahubiri Ya Yohana Mbatizaji
(Mathayo 3:1-12; Luka 3:1-8; Yohana 1:19-28)
1 aMwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.2 bKama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:
“Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,
atakayetengeneza njia mbele yako”:
3 c“sauti ya mtu aliaye nyikani.
‘Itengenezeni njia ya Bwana,
yanyoosheni mapito yake.’ ”
4 dYohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 eWatu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. 6 fYohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 7 gNaye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. 8 hMimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”
Ubatizo Wa Yesu
(Mathayo 3:13-17; Luka 3:21-22)
9 iWakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani. 10 jYesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua. 11 kNayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”Majaribu Ya Yesu
(Mathayo 4:1-11; Luka 4:1-13)
12 lWakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani, 13 mnaye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia.Yesu Aanza Kuhubiri
14 nBaada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu, 15 oakisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”Yesu Awaita Wanafunzi Wanne
(Mathayo 4:12-22; Luka 4:14-15; 5:1-11)
16 pYesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. 17 qYesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 18 rMara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.19 sAlipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20Papo hapo akawaita, nao wakamwacha Zebedayo baba yao kwenye mashua pamoja na watumishi wa kuajiriwa, nao wakamfuata Yesu.
Yesu Amtoa Pepo Mchafu
(Luka 4:31-37)
21 tWakaenda mpaka Kapernaumu. Ilipofika siku ya Sabato, mara Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha. 22 uWatu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana aliwafundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. 23 vWakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, 24 wnaye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”25 xLakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26 yYule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.
27 zWatu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” 28 aaSifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.
Yesu Amponya Mama Mkwe Wa Simoni
(Mathayo 8:14-15; Luka 4:38-39)
29 abMara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. 31 acHivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.Yesu Aponya Wengi
(Mathayo 8:16-17; Luka 4:40-41)
32 adJioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34 aeYesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.Yesu Aenda Galilaya
(Luka 4:42-44)
35 afAlfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba. 36 agSimoni na wenzake wakaenda kumtafuta, 37nao walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta!”38 ahYesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hicho ndicho nilichokuja kukifanya.” 39 aiKwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.
Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma
(Mathayo 8:1-4; Luka 5:12-16)
40 ajMtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”41Yesu, akiwa amejawa na huruma, akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” 42Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. 43 akBaada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake 44 alakimwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” 45 amLakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi lakini alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.
Copyright information for
SwhNEN