‏ Nahum 3

Ole Wa Ninawi

1 aOle wa mji umwagao damu,
uliojaa uongo,
umejaa nyara,
usiokosa kuwa na vitu vya kuteka nyara.
2 bKelele za mijeledi,
vishindo vya magurudumu,
farasi waendao mbio
na mshtuo wa magari ya vita!
3Wapanda farasi wanaenda mbio,
panga zinameremeta,
na mikuki inangʼaa!
Majeruhi wengi,
malundo ya maiti,
idadi kubwa ya miili isiyohesabika,
watu wanajikwaa juu ya mizoga:
4 cyote haya kwa sababu ya wingi wa tamaa za kahaba,
anayeshawishi, bibi wa mambo ya uchawi,
anayewatia utumwani mataifa kwa ukahaba wake
na pia jamaa za watu kwa ulozi wake.

5 d Bwana Mwenye Nguvu Zote anasema,
“Mimi ni kinyume na ninyi.
Nitafunika uso wako kwa gauni lako.
Nitaonyesha mataifa uchi wako
na falme aibu yako.
6 eNitakutupia uchafu,
nitakufanyia dharau
na kukufanya kioja.
7 fWote wanaokuona watakukimbia na kusema,
‘Ninawi ipo katika kuangamia:
ni nani atakayeomboleza kwa ajili yake?’
Nitampata wapi yeyote wa kukufariji?”

8 gJe, wewe ni bora kuliko No-Amoni,
uliopo katika Mto Naili,
uliozungukwa na maji?
Mto ulikuwa kinga yake,
nayo maji yalikuwa ukuta wake.
9 hKushi
Kushi ni Ethiopia.
na Misri walikuwa nguvu zake zisizo na mpaka;
Putu na Libia walikuwa miongoni mwa wale walioungana naye.
10 jHata hivyo alichukuliwa mateka
na kwenda uhamishoni.
Watoto wake wachanga walivunjwa vunjwa vipande
kwenye mwanzo wa kila barabara.
Kura zilipigwa kwa watu wake wenye heshima,
na watu wake wote wakuu walifungwa kwa minyororo.
11 kWewe pia utalewa;
utakwenda mafichoni
na kutafuta kimbilio kutoka kwa adui.

12 lNgome zako zote ni kama mitini
yenye matunda yake ya kwanza yaliyoiva;
wakati inapotikiswa,
tini huanguka kwenye kinywa chake alaye.
13 mTazama vikosi vyako:
wote ni wanawake!
Malango ya nchi yako
yamekuwa wazi kwa adui zako;
moto umeteketeza mapingo yake.

14 nTeka maji kwa ajili ya kuzingirwa kwako,
imarisha ulinzi wako,
Ufanyie udongo wa mfinyanzi kazi,
yakanyage matope,
karabati tanuru la kuchomea matofali!
15 oHuko moto utakuteketeza,
huko upanga utakuangusha chini
na kama vile panzi, watakumaliza.
Ongezeka kama panzi,
ongezeka kama nzige!
16 pUmeongeza idadi ya wafanyabiashara wako
mpaka wamekuwa wengi kuliko nyota za angani,
lakini kama nzige wanaacha nchi tupu
kisha huruka na kwenda zake.
17 qWalinzi wako ni kama nzige,
maafisa wako ni kama makundi ya nzige
watuao kwenye kuta wakati wa siku ya baridi:
lakini wakati jua linapotokea wanaruka kwenda zao,
na hakuna ajuaye waendako.

18 rEe mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wanasinzia;
wakuu wako wanalala chini mavumbini kupumzika.
Watu wako wametawanyika juu ya milima
bila kuwa na mtu yeyote wa kuwakusanya.
19 sHakuna kitu kinachoweza kuponya jeraha lako;
jeraha lako ni la kukuua.
Kila anayesikia habari zako,
hupiga makofi kwa kuanguka kwako,
kwa kuwa ni nani ambaye hajaguswa
na ukatili wako usio na mwisho?
Copyright information for SwhNEN