‏ Numbers 21

Nchi Ya Aradi Yaangamizwa

1 aMfalme wa Kikanaani wa Aradi aliyeishi huko Negebu aliposikia kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, aliwashambulia Waisraeli na kuwateka baadhi yao. 2 bNdipo Israeli akaweka nadhiri hii kwa Bwana: “Ikiwa utawatia watu hawa mikononi mwetu, tutaiangamiza kabisa miji yao.” 3 cBwana akasikiliza ombi la Waisraeli, naye akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Wakawaangamiza kabisa na miji yao; hivyo mahali pale pakaitwa Horma.
Horma maana yake Maangamizi.


Nyoka Wa Shaba

4 eWaisraeli wakasafiri kutoka mlima Hori kupitia njia inayoelekea Bahari ya Shamu,
Yaani Bahari Nyekundu au Bahari ya Mafunjo (ona 14:25).
kuizunguka Edomu. Lakini watu wakakosa uvumilivu njiani,
5 gwakamnungʼunikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini umetupandisha kutoka Misri ili tufe jangwani? Hakuna mkate! Hakuna maji! Nasi tunachukia sana chakula hiki duni!”

6 hNdipo Bwana akapeleka nyoka wenye sumu katikati yao; wakawauma watu, nao Waisraeli wengi wakafa. 7 iWatu wakamjia Mose na kusema, “Tumetenda dhambi wakati tuliponena dhidi ya Bwana na dhidi yako. Mwombe Bwana ili atuondolee hawa nyoka.” Hivyo Mose akawaombea hao watu.

8 j Bwana akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti; yeyote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.” 9 kKwa hiyo Mose akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu yeyote aliumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.

Safari Kwenda Moabu

10 lWaisraeli waliendelea na safari yao na wakapiga kambi huko Obothi. 11 mKisha wakaondoka Obothi na kupiga kambi huko Iye-Abarimu, katika jangwa linalotazamana na Moabu kuelekea mawio ya jua. 12 nKutoka hapo waliendelea mbele wakapiga kambi kwenye Bonde la Zeredi. 13 oWakasafiri kutoka hapo na kupiga kambi kando ya Mto Arnoni, ambao uko katika jangwa lililoenea hadi nchi ya Waamori. Arnoni ni mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori. 14 pNdiyo sababu Kitabu cha Vita vya Bwana kinasema:

“…Mji wa Wahebu nchini Seifa na mabonde
ya Arnoni,
15 qna miteremko ya mabonde
inayofika hadi mji wa Ari
na huelekea mpakani mwa Moabu.”
16 rKutoka hapo waliendelea mbele hadi kisima cha Beeri; kwenye kisima ambacho Bwana alimwambia Mose, “Wakusanye watu pamoja, nami nitawapa maji.”

17 sKisha Israeli akaimba wimbo huu:

“Bubujika, ee kisima!
Imba kuhusu maji,
18kuhusu kisima ambacho kilichimbwa na wakuu,
ambacho watu mashuhuri walikifukua,
watu mashuhuri wakiwa na fimbo za utawala na bakora.”
Kisha wakatoka jangwani kwenda Matana,
19kutoka Matana wakafika Nahalieli, kutoka Nahalieli wakafika Bamothi, 20 tna kutoka Bamothi wakafika kwenye bonde lililoko Moabu, mahali ambapo kilele cha Pisga kinatazamana na nyika.

Kushindwa Kwa Sihoni Na Ogu

(Kumbukumbu 2:26–3:11)

21 uIsraeli akawatuma wajumbe kumwambia Sihoni mfalme wa Waamori:

22 v“Uturuhusu tupite katika nchi yako. Hatutageuka kando kwenda katika mashamba au mashamba ya mizabibu, ama kunywa maji kutoka kisima chochote. Tutasafiri kwenye njia kuu ya mfalme hata tutakapokuwa tumekwisha kupita katika nchi yako.”

23 wLakini Sihoni hakumruhusu Israeli apite katika nchi yake. Alilikutanisha jeshi lake lote, wakaondoka kwenda jangwani ili kupigana na Israeli. Alipofika huko Yahazi, akapigana na Israeli. 24 xHata hivyo, Israeli alimshinda kwa upanga na kuiteka ardhi yake kutoka Arnoni mpaka Yaboki, lakini ni hadi kufikia nchi ya Waamoni tu, kwa sababu mipaka yake ilikuwa imezungushwa ukuta. 25 yIsraeli akaiteka miji yote ya Waamori na kuikalia, pamoja na Heshboni na makazi yote yanayoizunguka. 26 zHeshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alikuwa amepigana dhidi ya mfalme wa Moabu aliyetangulia na akawa amechukua ardhi yake yote mpaka Arnoni.

27Ndiyo sababu watunga mashairi husema:

“Njoo Heshboni na ujengwe tena;
mji wa Sihoni na ufanywe upya.

28 aa“Moto uliwaka kutoka Heshboni,
mwali wa moto kutoka mji wa Sihoni.
Uliteketeza Ari ya Moabu,
raiya wa mahali pa Arnoni palipoinuka.
29 abOle wako, ee Moabu!
Umeharibiwa, enyi watu wa Kemoshi!
Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi,
na binti zake kama mateka
kwa Mfalme Sihoni wa Waamori.

30 ac“Lakini tumewashinda;
Heshboni umeharibiwa hadi Diboni.
Tumebomoa hadi kufikia Nofa,
ulioenea hadi Medeba.”
31 adKwa hiyo Israeli akaishi katika nchi ya Waamori.

32 aeBaada ya Mose kutuma wapelelezi kwenda mji wa Yazeri, Waisraeli waliteka viunga vya mji huo na kuwafukuza Waamori waliokuwa wanaishi huko. 33 afKisha wakageuka na kwenda katika njia inayoelekea Bashani, naye Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote wakatoka kupigana nao huko Edrei.

34 ag Bwana akamwambia Mose, “Usimwogope Ogu, kwa sababu nimeshamkabidhi mikononi mwako, pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Mtendee kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”

35 ahKwa hiyo wakamuua, pamoja na wanawe na jeshi lake lote, bila ya kumwacha hata mtu mmoja hai. Nao wakaimiliki nchi yake.

Copyright information for SwhNEN