2 Chronicles 13
Abiya Mfalme Wa Yuda
(1 Wafalme 15:1-8)
1Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu, Abiya akawa mfalme wa Yuda, 2 anaye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka, binti Urieli wa Gibea. Basi kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu. 3Abiya aliingia vitani na jeshi la watu 400,000 wenye uwezo wa kupigana, naye Yeroboamu akapanga jeshi dhidi ya Abiya akiwa na jeshi la watu 800,000 wenye uwezo. 4 bAbiya akasimama juu ya Mlima Semaraimu, katika nchi ya vilima ya Efraimu, naye akasema, “Yeroboamu na Israeli yote, nisikilizeni mimi! 5 cHamfahamu kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi na wazao wake ufalme juu ya Israeli milele kwa Agano la chumvi? 6 dHata hivyo Yeroboamu mwana wa Nebati afisa wa Sulemani mwana wa Daudi, aliasi dhidi ya bwana wake. 7 eBaadhi ya watu wasiofaa kitu, wabaya kabisa walimkusanyikia na kumpinga Rehoboamu mwana wa Sulemani alipokuwa kijana mdogo asiyekuwa na uamuzi, asiye na nguvu za kuweza kupingana nao. 8 f g“Hata sasa unapanga kupingana na ufalme wa Bwana ambao uko mikononi mwa wazao wa Daudi. Kweli ninyi ni jeshi kubwa nanyi mnazo ndama za dhahabu Yeroboamu alizozitengeneza kuwa miungu yenu. 9 hLakini je, hamkuwafukuza makuhani wa Bwana, wana wa Haruni na Walawi na kujifanyia makuhani wenu wenyewe kama yafanyavyo mataifa ya nchi nyingine? Yeyote anayekuja kujiweka wakfu akiwa na ndama dume na kondoo dume saba aweza kuwa kuhani wa kile ambacho ni miungu kwenu. 10“Lakini kwetu sisi, Bwana ndiye Mungu wetu, wala hatujamwacha. Makuhani wanaomtumikia Bwana ni wana wa Haruni, nao Walawi wakiwasaidia. 11 iKila asubuhi na jioni wao hutoa sadaka za kuteketezwa na kufukiza uvumba wa harufu nzuri kwa Bwana. Wao huweka mikate juu ya meza safi kwa taratibu za kiibada na kuwasha taa kwenye kinara cha dhahabu kila jioni. Sisi tunazishika kanuni za Bwana Mwenyezi Mungu wetu. Lakini ninyi mmemwacha Mungu. 12 jMungu yu pamoja nasi, yeye ndiye kiongozi wetu. Makuhani wake wakiwa na tarumbeta zao watapiga baragumu ya vita dhidi yenu. Watu wa Israeli, msipigane dhidi ya Bwana, Mungu wa baba zenu, kwa maana hamtashinda.” 13 kBasi Yeroboamu alikuwa ametuma jeshi kuzunguka nyuma ya Yuda ili kwamba akiwa mbele ya Yuda, jeshi liwavizie kwa nyuma. 14 lBasi Yuda wakageuka na kuona kwamba wanashambuliwa mbele na nyuma. Ndipo wakamlilia Bwana. Makuhani wakapiga tarumbeta zao, 15 mnao watu wa Yuda wakapaza sauti ya kilio cha vita. Katika kupiga kelele za vita, Mungu akawafukuza Yeroboamu na Israeli wote mbele ya Mfalme Abiya na Yuda. 16 nWaisraeli wakakimbia mbele ya Yuda, naye Mungu akawatia Israeli mikononi mwao. 17Abiya na watu wake wakawachinja kwa machinjo makuu, hata wakawepo majeruhi 500,000 miongoni mwa watu wenye uwezo wa Israeli. 18 oWatu wa Israeli walitiishwa katika tukio lile, nao watu wa Yuda wakawa washindi kwa sababu walimtegemea Bwana, Mungu wa baba zao. 19 pAbiya akamfuatia Yeroboamu na kuteka miji ya Betheli, Yeshana na Efroni kutoka kwake, pamoja na vijiji vinavyoizunguka miji hiyo. 20 qYeroboamu hakupata nguvu tena wakati wa utawala wa Abiya. Naye Bwana akampiga Yeroboamu akafa. 21Lakini Abiya akapata nguvu. Alioa wanawake kumi na wanne na alikuwa na wana ishirini na wawili na binti kumi na sita. 22 rMatukio mengine ya utawala wa Abiya, pamoja na mambo aliyofanya na aliyosema, yameandikwa katika kitabu cha maelezo cha nabii Ido.
Copyright information for
SwhKC