‏ 2 Samuel 18

Kifo Cha Absalomu

1Daudi akakusanya watu aliokuwa nao na kuweka majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia. 2 aDaudi akatuma vikosi vya askari: theluthi moja ilikuwa chini ya amri ya Yoabu, theluthi ya pili chini ya Abishai mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya Itai, Mgiti. Mfalme akaviambia vikosi, “Hakika mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nanyi.”

3 bLakini watu wakasema, “Haikupasi kwenda, ikiwa sisi tutalazimika kukimbia, wao hawatatujali. Hata kama nusu yetu tukifa hawatajali, lakini wewe una thamani ya watu kama sisi kumi elfu. Ingekuwa bora zaidi kwako basi kutupatia msaada kutoka mjini.”

4Mfalme akajibu, “Nitafanya lolote linaloonekana jema zaidi kwenu.”

Kwa hiyo mfalme akasimama kando ya lango wakati watu wote wakitoka nje kwa makundi ya mamia na maelfu.
5Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Kuweni wapole kwa kijana Absalomu kwa ajili yangu.” Vikosi vyote vikasikia mfalme akitoa amri kwa kila jemadari kumhusu Absalomu.

6 cJeshi likatoka kwenda kwenye uwanja wa vita kupigana na Israeli, hivyo vita vikapiganwa katika msitu wa Efraimu. 7 dHuko jeshi la Israeli likashindwa na watu wa Daudi, siku hiyo majeruhi walikuwa wengi kiasi cha watu ishirini elfu. 8Vita vikaenea nchi nzima, watu wengi zaidi wakifia msituni siku hiyo kuliko waliouawa kwa upanga.

9 eBasi ikawa Absalomu alikutana na watu wa Daudi. Yeye alikuwa amepanda nyumbu wake, naye nyumbu alipopita chini ya matawi yaliyosongana ya mwaloni mkubwa, kichwa cha Absalomu kilinaswa kwenye mti. Akaachwa akining’inia hewani, wakati nyumbu aliyekuwa amempanda aliendelea kwenda.

10Mmojawapo wa wale watu alipoona, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akining’inia kwenye mti wa mwaloni.”

11 fYoabu akamwambia huyo mtu, “Nini! Ulimwona Absalomu? Kwa nini hukumpiga papo hapo mpaka chini? Ndipo ningekupa shekeli kumi
Shekeli kumi za fedha ni sawa na gramu 115.
za fedha na mkanda wa askari shujaa.”

12Lakini huyo mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepimiwa shekeli 1,000
Shekeli 1,000 za fedha ni sawa na kilo 11.5.
mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’
13 iNami kama ningekuwa nimemtendea kwa hila, na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme, wewe mwenyewe ungejitenga nami.”

14 jYoabu akasema, “Mimi sitapoteza muda hapa pamoja nawe.” Hivyo akachukua mikuki mitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu nayo moyoni alipokuwa angali hai akining’inia katika ule mwaloni. 15 kNao wabeba silaha kumi wa Yoabu wakamzunguka Absalomu, wakampiga na kumuua.

16 lKisha Yoabu akapiga tarumbeta, navyo vikosi vikaacha kuwafuata Israeli, kwa maana Yoabu aliwasimamisha. 17 mWakamchukua Absalomu, wakamtupa katika shimo kubwa huko msituni na kulundika lundo kubwa la mawe juu yake. Huko nyuma, Waisraeli wote wakakimbilia nyumbani kwao.

18 nWakati wa uhai wa Absalomu alikuwa amechukua nguzo na kuisimamisha katika Bonde la Mfalme, kwa maana alifikiri, “Sina mwana atakayeendeleza kumbukumbu ya jina langu.” Akaita nguzo hiyo kwa jina lake mwenyewe. Nayo inaitwa Mnara wa Ukumbusho wa Absalomu mpaka leo.

Daudi Aomboleza Kifo Cha Absalomu

19 oBasi Ahimaasi mwana wa Sadoki akasema, “Niruhusu mimi nikimbie na kumpelekea mfalme habari kwamba Bwana amemwokoa mfalme kutoka mikononi mwa adui zake.”

20Yoabu akamwambia Ahimaasi, “Leo si wewe utakayepeleka habari. Unaweza kupeleka habari wakati mwingine, lakini leo haikupasi kupeleka, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa.”

21Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja Mkushi, “Nenda, ukamwambie mfalme kile ulichoona.” Mkushi akasujudu mbele ya Yoabu akaondoka mbio.

22Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia tena Yoabu, “Liwalo na liwe, tafadhali niruhusu nikimbie nyuma ya huyo Mkushi.”

Lakini Yoabu akajibu, “Mwanangu, mbona wataka kwenda? Wewe huna habari yoyote itakayokupa tuzo.”

23Ahimaasi akasema, “Liwalo na liwe, nataka kukimbia.”

Kwa hiyo Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia!” Ndipo Ahimaasi akakimbia kufuata njia ya kupitia tambarare, akafika kabla ya huyo Mkushi.

24 pWakati Daudi alipokuwa ameketi kati ya lango la ndani na la nje, mlinzi akapanda juu ya paa la lango kupitia ukutani. Alipotazama nje, akaona mtu mmoja akikimbia peke yake. 25Mlinzi akampazia mfalme sauti na kumpa taarifa.

Mfalme akasema, “Ikiwa yuko peke yake, lazima atakuwa na habari njema.” Naye yule mtu akazidi kusogea karibu.

26 qKisha mlinzi akaona mtu mwingine anakuja akikimbia, akamwita bawabu, “Tazama, mtu mwingine anakuja akikimbia peke yake!”

Mfalme akasema, “Lazima atakuwa analeta habari njema pia.”

27 rMlinzi akasema, “Ninaona kuwa yule wa kwanza anakimbia kama Ahimaasi mwana wa Sadoki.”

Mfalme akasema, “Yeye ni mtu mwema. Analeta habari njema.”

28Ndipo Ahimaasi akamwita mfalme, akasema, “Mambo yote ni mema!” Akasujudu mbele ya mfalme uso wake mpaka ardhini, akasema, “Ahimidiwe Bwana Mwenyezi Mungu wako! Yeye aliyewatoa watu wale walioinua mikono yao dhidi ya mfalme bwana wangu.”

29Mfalme akauliza, “Je, huyo kijana Absalomu yuko salama?”

Ahimaasi akajibu, “Kulikuwa na machafuko mengi mara tu Yoabu alipokuwa anataka kumtuma mtumishi wa mfalme pamoja nami mtumishi wako, lakini sijui ilikuwa nini?”

30Mfalme akasema, “Simama kando na usubiri hapa.” Basi akasogea kando na kusimama hapo.

31 sNdipo huyo Mkushi akawasili na kusema, “Mfalme bwana wangu, sikia habari njema! Leo Bwana amekuokoa kutoka kwa wale wote walioinuka dhidi yako.”

32 tMfalme akamuuliza huyo Mkushi, “Je, kijana Absalomu yuko salama?”

Huyo Mkushi akajibu, “Adui wa mfalme bwana wangu na wote wale walioinuka kukudhuru na wawe kama huyo kijana.”

33 uMfalme akatetemeka. Akapanda chumbani juu kupitia langoni akilia. Alipokuwa akienda, akasema, “Ee mwanangu Absalomu! Mwanangu, mwanangu Absalomu! Laiti ningekufa badala yako: Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”
Copyright information for SwhKC