Genesis 48
Manase Na Efraimu
1Baada ya muda Yusufu akaambiwa kwamba, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu, pamoja naye. 2Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yusufu amekujia kukuona,” Israeli akakusanya nguvu zake, akaketi kitandani. 3Yakobo akamwambia Yusufu, “Mwenyezi Mungu ▼▼ Mwenyezi Mungu hapa ni jina la Kiebrania, El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).
alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani, huko akanibariki, 4naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na kuongezeka hesabu yako, nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele wewe na wazao wako baada yako.’ 5“Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa ni wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu. 6Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao. 7Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, katika huzuni yangu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tungali tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrathi. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrathi” (yaani Bethlehemu). 8Wakati Israeli alipowaona wana wa Yusufu, akauliza, “Hawa ni nani?” 9Yusufu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.” Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.” 10Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yusufu akawaleta wanawe karibu na baba yake, Israeli akawabusu na akawakumbatia. 11Israeli akamwambia Yusufu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.” 12Ndipo Yusufu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli naye akasujudu hadi nchi. 13Yusufu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. 14Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa ndiye mdogo, na mkono wake wa kushoto akaukatisha, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza. 15Ndipo akambariki Yusufu akisema, “Mungu ambaye baba zanguIbrahimu na Isaka walimtii,
Mungu ambaye amekuwa mchungaji
wa maisha yangu yote mpaka leo hii,
16 Malaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote,
yeye na awabariki vijana hawa.
Na waitwe kwa jina langu
na kwa majina ya baba zangu Ibrahimu na Isaka,
wao na waongezeke kwa wingi
katika dunia.”
17Yusufu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase. 18Yusufu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.” 19Lakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.” 20Akawabarikia siku ile na kusema, “Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii:
‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ”
Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase. 21Ndipo Israeli akamwambia Yusufu, “Mimi ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. 22Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”
Copyright information for
SwhKC