‏ Luke 6

Bwana Wa Sabato

(Mathayo 12:1-8; Marko 2:23-28)

1 aIkawa siku moja ya Sabato Isa alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, nao wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake. 2 bBaadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo yasiyo halali kufanywa siku ya Sabato?”

3 cIsa akawajibu, “Je, ninyi hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa? 4 dAliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua na kuila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.” 5 eIsa akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Mtu Aliyepooza Mkono Aponywa

(Mathayo 12:9-14; Marko 3:1-6)

6 fIkawa siku nyingine ya Sabato, Isa aliingia ndani ya sinagogi na akawa anafundisha. Huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. 7 gMafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Isa. Kwa hivyo wakawa wanamwangalia sana ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato. 8 hLakini Isa alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka usimame mbele ya watu wote.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote.

9Ndipo Isa akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato? Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuyaangamiza?”

10 iAkawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyoosha mkono wako!” Akaunyoosha na mkono wake ukaponywa kabisa. 11 jWale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao ni nini watakachomtendea Isa.

Isa Achagua Mitume Kumi Na Wawili

(Mathayo 10:1-4; Marko 3:13-19)

12 kIkawa katika siku hizo Isa alikwenda mlimani kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu. 13 lKulipopambazuka, akawaita wanafunzi wake, naye akachagua kumi na wawili, ambao pia aliwaita mitume: 14 mSimoni aliyemwita Petro, Andrea nduguye, Yakobo, Yohana, Filipo, Bartholomayo, 15 nMathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni aliyeitwa Zelote, 16Yuda mwana wa Yakobo, na Yuda Iskariote ambaye alikuwa msaliti.

Isa Aponya Wengi

(Mathayo 4:23-25)

17 oAkashuka pamoja nao, akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Uyahudi, kutoka Yerusalemu, na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni. 18 pWalikuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya. 19 qWatu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote.

Baraka Na Ole

(Mathayo 5:1-12)

20 rAkawatazama wanafunzi wake, akasema: “Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,
kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu.

21 sMmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,
kwa sababu mtashibishwa.
Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,
kwa sababu mtacheka.

22 tMmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,
watakapowatenga na kuwatukana
na kulikataa jina lenu kama neno ovu,
kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

23 u“Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.
24 v“Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri,
kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.

25 wOle wenu ninyi mlioshiba sasa,
maana mtaona njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
maana mtaomboleza na kulia.

26 xOle wenu watu watakapowasifu,
kwani ndivyo baba zao walivyowasifu
manabii wa uongo.

Wapendeni Adui Zenu

(Mathayo 5:38-48)

27 y“Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. 28 zWabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. 29 aaKama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyang’anya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. 30 abMpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. 31 acWatendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.

32 ad“Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao. 33Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. 34 aeTena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 afLakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. 36 agKuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

Kuwahukumu Wengine

(Mathayo 7:1-5)

37 ah“Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. 38 aiWapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

39 ajPia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni? 40 akMwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.

41 al“Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? 42 amUtawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.

Mti Na Mazao Yake

(Mathayo 7:16-20; Marko 12:33-35)

43 an“Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri. 44 aoKila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba, wala zabibu kwenye michongoma. 45 apVivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka kwenye hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo maovu kutoka kwenye hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake.

Mjenzi Mwenye Busara Na Mjenzi Mpumbavu

(Mathayo 7:24-27)

46 aq“Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia? 47 arNitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda. 48Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yaliipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri. 49Lakini yeye anayesikia maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”
Copyright information for SwhKC