Jeremiah 40:1-6

Yeremia Aachiwa Huru

1 aNeno likamjia Yeremia kutoka kwa Bwana baada ya Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli. 2 bKiongozi wa walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “Bwana Mwenyezi Mungu wako aliamuru maafa haya kwa mahali hapa. 3 cSasa Bwana ameyaleta haya, amefanya sawasawa na vile alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya Bwana na hamkumtii. 4 dLakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Twende pamoja mpaka Babeli ikiwa unataka, nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.” 5 eLakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.”

Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake.
6 fKwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.

Gedalia Auawa

(2 Wafalme 25:22-26)

Copyright information for SwhKC