2 Corinthians 8
Kutoa Kwa Ukarimu
1 aBasi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia. 2 bPamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu. 3 cKwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe, 4 dwakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu. 5Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu. 6 eKwa hiyo tulimsihi Tito, kwa kuwa ndiye alianzisha jambo hili, akamilishe tendo hili la neema kwa upande wenu. 7 fLakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa.8 gSiwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine. 9 hKwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.
10 iUshauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu juu ya jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo. 11 jSasa ikamilisheni kazi hii kwa shauku kama mlivyoanza, jitoleeni kulingana na uwezo wenu. 12 kKwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.
13Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano. 14 lKwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. 15 mNdipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”
Tito Atumwa Korintho
16 nNinamshukuru Mungu ambaye amemtia Tito moyo wa kuwajali ninyi kama mimi ninavyowajali. 17 oSi kwamba Tito amekubali tu ombi letu, bali anakuja kwenu akiwa na shauku kuliko wakati mwingine, tena kwa hiari yake mwenyewe. 18 pNasi tunamtuma pamoja naye ndugu ambaye anasifiwa na makanisa yote kwa huduma yake ya kuhubiri Injili. 19 qZaidi ya hayo, alichaguliwa na makanisa ili asafiri pamoja nasi tulipokuwa tunapeleka matoleo ya ukarimu, kwa ajili ya utukufu wa Bwana mwenyewe, na ili kuonyesha hisani yetu kuwasaidia. 20Tunataka kuepuka lawama yoyote kuhusu jinsi tunavyosimamia matoleo haya ya ukarimu. 21 rKwa kuwa tunakusudia kufanya kile kilicho haki si machoni mwa Bwana peke yake, bali pia machoni mwa watu wengine.22Pamoja nao, tunamtuma ndugu yetu ambaye mara kwa mara ametuthibitishia kwa njia nyingi kwamba ana shauku, naam, zaidi sana sasa kwa sababu analo tumaini kuu kwenu. 23 sKwa habari ya Tito, yeye ni mwenzangu na mtendakazi pamoja nami miongoni mwenu. Kwa habari za ndugu zetu, wao ni wawakilishi wa makanisa, na utukufu kwa Kristo. 24 tKwa hiyo waonyesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, mbele ya makanisa, ili yapate kuona.
Copyright information for
SwhNEN