‏ Deuteronomy 15

Mwaka Wa Kufuta Madeni

(Walawi 25:1-7)

1 aKila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. 2Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Bwana wa kufuta madeni umetangazwa. 3 bUnaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. 4 cHata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, 5 dikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. 6 eKwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi.

7 fIkiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 gAfadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. 9 hJihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. 10 iMpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. 11 jSiku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu.

Kuwaacha Huru Watumwa

(Kutoka 21:1-18)

12 kKama Mwebrania mwenzako, mwanaume au mwanamke, akijiuza kwako na kukutumikia miaka sita, katika mwaka wa saba ni lazima umwache aende zake akiwa huru. 13Nawe wakati utakapomwachia usimwache aende mikono mitupu. 14 lMpe kwa uhuru kutoka zizi lako la kondoo na mbuzi, kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka na kutoka mashinikizo yako ya kukamulia divai. Mpe kama vile ambavyo Bwana Mungu wako alivyokubariki. 15 mKumbukeni kuwa ninyi mlikuwa watumwa huko Misri naye Bwana Mungu wenu aliwakomboa. Ndiyo sababu nimewapa agizo hili leo.

16 nLakini mtumishi wako akikuambia, “Sitaki kukuacha,” kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako naye anaridhika nawe, 17ndipo utachukua chuma kidogo utoboe sikio lake mpaka hicho chuma kiingie kwenye ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako wa maisha. Ufanye vivyo hivyo kwa mtumishi wa kike.

18 oUsifikiri kuwa kuna ugumu kumwacha mtumishi wako huru, kwa sababu utumishi wake kwako kwa miaka hii sita umekuwa wa thamani mara mbili ya ujira wa mtumishi wa kuajiriwa. Naye Bwana Mungu wenu atakubarikia kwa kila kitu utakachofanya.

Wazaliwa Wa Kwanza Wa Wanyama

19 pWekeni wakfu kwa Bwana Mungu wenu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa makundi yenu ya ngʼombe na ya mbuzi na kondoo. Maksai walio wazaliwa wa kwanza msiwafanyize kazi, wala msinyoe manyoya ya wazaliwa wa kwanza wa kondoo. 20 qKila mwaka ninyi na jamaa zenu mtapaswa kuwala mbele za Bwana Mungu wenu pale mahali atakapopachagua. 21 rKama mnyama ana dosari, akiwa ni kilema au kipofu au kama ana kilema kibaya, kamwe usimtoe dhabihu kwa Bwana Mungu wenu. 22 sItawapasa kumla ninyi wenyewe katika miji yenu. Wote wasio safi na walio safi kwa desturi za kiibada mwaweza kula kama vile mnavyokula paa au kulungu. 23 tLakini kamwe msinywe damu; imwageni ardhini kama maji.

Copyright information for SwhNEN