‏ Isaiah 51

Wokovu Wa Milele Kwa Sayuni

1 a“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki
na mnaomtafuta Bwana:
Tazameni mwamba ambako mlichongwa,
na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;
2 bmwangalieni Abrahamu, baba yenu,
na Sara, ambaye aliwazaa.
Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu,
nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.
3 cHakika Bwana ataifariji Sayuni,
naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote;
atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni,
nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya Bwana.
Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake,
shukrani na sauti za kuimba.

4 d“Nisikilizeni, watu wangu;
nisikieni, taifa langu:
Sheria itatoka kwangu;
haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.
5 eHaki yangu inakaribia mbio,
wokovu wangu unakuja,
nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.
Visiwa vitanitegemea
na kungojea mkono wangu kwa matumaini.
6 fInueni macho yenu mbinguni,
mkaitazame dunia chini;
mbingu zitatoweka kama moshi,
dunia itachakaa kama vazi,
na wakazi wake kufa kama mainzi.
Bali wokovu wangu utadumu milele,
haki yangu haitakoma kamwe.

7 g“Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa,
ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu:
Msiogope mashutumu ya wanadamu
wala msitiwe hofu na matukano yao.
8 hKwa maana nondo atawala kama vazi,
nao funza atawatafuna kama sufu.
Lakini haki yangu itadumu milele,
wokovu wangu kwa vizazi vyote.”

9 iAmka, Amka! Jivike nguvu,
ewe mkono wa Bwana,
Amka, kama siku zilizopita,
kama vile vizazi vya zamani.
Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande,
uliyemchoma yule joka?
10 jSi ni wewe uliyekausha bahari,
maji ya kilindi kikuu,
uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari
ili waliokombolewa wapate kuvuka?
11 kWale waliolipiwa fidia na Bwana watarudi.
Wataingia Sayuni wakiimba;
furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.
Furaha na shangwe zitawapata,
huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.

12 l“Mimi, naam mimi,
ndimi niwafarijie ninyi.
Ninyi ni nani hata kuwaogopa
wanadamu wanaokufa,
wanadamu ambao ni majani tu,
13 mkwamba mnamsahau Bwana Muumba wenu,
aliyezitanda mbingu
na kuiweka misingi ya dunia,
kwamba mnaishi katika hofu siku zote
kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu,
ambaye nia yake ni kuangamiza?
Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?
14 nWafungwa waliojikunyata kwa hofu
watawekwa huru karibuni;
hawatafia kwenye gereza lao,
wala hawatakosa chakula.
15 oKwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume:
Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.
16 pNimeweka maneno yangu kinywani mwako
na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu:
Mimi niliyeweka mbingu mahali pake,
niliyeweka misingi ya dunia,
niwaambiaye Sayuni,
‘Ninyi ni watu wangu.’ ”

Kikombe Cha Ghadhabu Ya Bwana

17 qAmka, amka!
Simama, ee Yerusalemu,
wewe uliyekunywa kutoka mkono wa Bwana
kikombe cha ghadhabu yake,
wewe uliyekunywa mpaka kufikia machujo yake,
kikombe kile cha kunywea
kiwafanyacho watu kuyumbayumba.
18 rKati ya wana wote aliowazaa
hakuwepo hata mmoja wa kumwongoza,
kati ya wana wote aliowalea
hakuwepo hata mmoja wa kumshika mkono.
19 sMajanga haya mawili yamekuja juu yako:
ni nani awezaye kukufariji?
Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga:
ni nani awezaye kukutuliza?
20 tWana wako wamezimia,
wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara,
kama swala aliyenaswa kwenye wavu.
Wamejazwa na ghadhabu ya Bwana
na makaripio ya Mungu wako.

21 uKwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa,
uliyelewa, lakini si kwa mvinyo.
22 v wHili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi wako,
Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake:
“Tazama, nimeondoa mkononi mwako
kikombe kilichokufanya uyumbayumbe;
kutoka kikombe hicho,
kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu,
kamwe hutakunywa tena.
23 x yNitakiweka mikononi mwa watesi wako,
wale waliokuambia,
‘Anguka kifudifudi
ili tuweze kutembea juu yako.’
Ukaufanya mgongo wako kama ardhi,
kama njia yao ya kupita.”
Copyright information for SwhNEN