‏ Leviticus 14:1-32

Kutakasa Kutoka Maambukizo Ya Magonjwa Ya Ngozi

1 Bwana akamwambia Mose, 2 a“Haya ndiyo masharti yamhusuyo mtu mgonjwa wakati wa kufanyiwa ibada ya utakaso wakati aletwapo kwa kuhani: 3Kuhani atakwenda kumchunguza nje ya kambi. Kama mtu huyo atakuwa amepona ugonjwa wake wa ngozi wa kuambukiza, 4 bkuhani ataagiza vitu vifuatavyo viletwe kwa ajili ya mtu atakayetakaswa: ndege wawili safi walio hai, mti wa mwerezi, kitani nyekundu, na hisopo. 5Kisha kuhani ataagiza kwamba mmoja wa ndege wale achinjwe kwenye chungu chenye maji safi. 6Kisha kuhani atamchukua ndege aliye hai na kumtumbukiza pamoja na mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo ndani ya damu ya yule ndege aliyechinjiwa kwenye maji safi. 7 cAtamnyunyizia yule mwenye ugonjwa wa kuambukiza maji hayo mara saba, na kumtangaza kuwa safi. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai aende zake kwenye mashamba.

8 d“Huyo mtu atakayetakaswa ni lazima afue nguo zake, anyoe nywele zake zote, na aoge kwa maji; ndipo atakapokuwa safi kwa desturi ya ibada. Baada ya hili anaweza kuingia kambini, lakini ni lazima akae nje ya hema lake kwa siku saba. 9 eSiku ya saba ni lazima anyoe nywele zake zote; yaani anyoe nywele za kichwa, ndevu zake, kope zake na nywele nyingine zote. Ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa safi.

10 f“Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi za efa
Sehemu tatu za kumi za efa ni sawa na kilo 3.
za unga laini uliochanganywa na mafuta, kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi moja
Logi ni kipimo cha ujazo ambacho ni sawa na lita 0.3.
ya mafuta.
11 iKuhani atakayemtangaza kuwa safi atahitaji kumkabidhi mgonjwa aliyepona pamoja na sadaka zake zote mbele za Bwana katika ingilio la Hema la Kukutania.

12 j“Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia, pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa. 13 kAtamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjiwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; nayo ni takatifu sana. 14 lKuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 15Kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, ayamimine kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto, 16na achovye kidole chake cha shahada cha mkono wake wa kuume kwenye mafuta yaliyoko kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho anyunyize mafuta hayo mara saba mbele za Bwana. 17 mKuhani atampaka yule anayetakaswa sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio lake la kuume, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia. 18 nKuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana.

19 o“Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa 20 pna kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi.

21 q“Hata hivyo, kama ni maskini na hawezi kupata vitu hivi, lazima achukue mwana-kondoo mmoja kama sadaka ya hatia ipate kuinuliwa ili kumfanyia upatanisho, pamoja na sehemu ya kumi ya efa
Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na lita 2.
ya unga laini uliochanganywa na logi moja ya mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka,
22 sna hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kile atakachoweza kupata, mmoja kwa sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa.

23“Katika siku ya nane, lazima avilete vitu hivyo kwa kuhani, kwa ajili ya kutakaswa kwake kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Bwana. 24 tKuhani atamchukua mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia, pamoja na ile logi ya mafuta ya kuinuliwa mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa. 25 uAtamchinja huyo mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia. Pia ataichukua sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, na aipake pia kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume wa huyo mtu, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 26Kuhani atamiminia sehemu ya mafuta kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto, 27na kwa kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume, atamnyunyizia yule anayetakaswa yale mafuta yaliyo kwenye kiganja chake mara saba mbele za Bwana. 28Atampaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake katika sehemu zote, kama alivyompaka damu ya sadaka ya hatia: yaani, kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 29Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki katika kiganja chake kwenye kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana. 30 vKisha atatoa dhabihu wale hua ama yale makinda ya njiwa ambayo mtu ataweza kuwapata, 31 wmmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya nafaka. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya yule anayetakaswa.”

32 xHaya ndiyo masharti kwa mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, na ambaye hana uwezo wa kutoa sadaka za kawaida kwa ajili ya kutakaswa kwake.

Copyright information for SwhNEN