‏ Psalms 78

Mungu Na Watu Wake

Utenzi wa Asafu.

1 aEnyi watu wangu, sikieni mafundisho yangu,
sikilizeni maneno ya kinywa changu.
2 bNitafungua kinywa changu kwa mafumbo,
nitazungumza mambo yaliyofichika, mambo ya kale:
3 cyale ambayo tuliyasikia na kuyajua,
yale ambayo baba zetu walituambia.
4 dHatutayaficha kwa watoto wao;
tutakiambia kizazi kijacho
matendo yastahiliyo sifa ya Bwana,
uweza wake, na maajabu aliyoyafanya.
5 eAliagiza amri kwa Yakobo
na akaweka sheria katika Israeli,
ambazo aliwaamuru baba zetu
wawafundishe watoto wao,
6 fili kizazi kijacho kizijue,
pamoja na watoto ambao watazaliwa,
nao pia wapate kuwaeleza watoto wao.
7 gNdipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu,
nao wasingesahau matendo yake,
bali wangalizishika amri zake.
8 hIli wasifanane na baba zao,
waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi,
ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwake,
ambao roho zao hazikumwamini.

9 iWatu wa Efraimu, ingawa walijifunga pinde,
walikimbia siku ya vita.
10 jHawakulishika agano la Mungu
na walikataa kuishi kwa sheria yake.
11 kWalisahau aliyokuwa ameyatenda,
maajabu aliyokuwa amewaonyesha.
12 lAlitenda miujiza machoni mwa baba zao,
huko Soani, katika nchi ya Misri.
13 mAliigawanya bahari akawapitisha,
alifanya maji yasimame imara kama ukuta.
14 nAliwaongoza kwa wingu mchana
na kwa nuru kutoka kwenye moto usiku kucha.
15 oAlipasua miamba jangwani
na akawapa maji tele kama bahari,
16 palitoa vijito kutoka kwenye jabali lililochongoka,
akayafanya maji yatiririke kama mito.

17 qLakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake,
wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana.
18 rKwa makusudi walimjaribu Mungu,
wakidai vyakula walivyovitamani.
19 sWalinena dhidi ya Mungu, wakisema,
“Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani?
20 tAlipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu,
vijito vikatiririka maji mengi.
Lakini je, aweza kutupa chakula pia?
Je, anaweza kuwapa watu wake nyama?”
21 u Bwana alipowasikia, alikasirika sana,
moto wake ukawa dhidi ya Yakobo,
na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli,
22 vkwa kuwa hawakumwamini Mungu,
wala kuutumainia ukombozi wake.
23 wHata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu
na kufungua milango ya mbingu,
24 xakawanyeshea mana ili watu wale;
aliwapa nafaka ya mbinguni.
25Watu walikula mkate wa malaika,
akawatumia chakula chote ambacho wangeliweza kula.
26 yAliachia upepo wa mashariki kutoka kwenye mbingu
na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake.
27 zAliwanyeshea nyama kama mavumbi,
ndege warukao kama mchanga wa pwani.
28Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao,
kuzunguka mahema yao yote.
29 aaWalikula na kusaza,
kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani.
30 abKabla hawajamaliza kula walichokitamani,
hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao,
31 achasira ya Mungu ikawaka juu yao,
akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao,
akiwaangusha vijana wa Israeli.

32 adLicha ya haya yote, waliendelea kutenda dhambi,
licha ya maajabu yake, hawakuamini.
33 aeKwa hiyo akamaliza siku zao katika ubatili
na miaka yao katika vitisho.
34 afKila mara Mungu alipowaua baadhi yao,
waliosalia walimtafuta,
walimgeukia tena kwa shauku.
35 agWalikumbuka kwamba Mungu alikuwa Mwamba wao,
kwamba Mungu Aliye Juu Sana alikuwa Mkombozi wao.
36 ahLakini walimdanganya kwa vinywa vyao,
wakisema uongo kwa ndimi zao,
37 aimioyo yao haikuwa thabiti kwake,
wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.
38 ajHata hivyo alikuwa na huruma,
alisamehe maovu yao
na hakuwaangamiza.
Mara kwa mara alizuia hasira yake,
wala hakuchochea ghadhabu yake yote.
39 akAlikumbuka kwamba wao walikuwa nyama tu,
upepo upitao ambao haurudi.

40 alMara ngapi walimwasi jangwani
na kumhuzunisha nyikani!
41 amWalimjaribu Mungu mara kwa mara,
wakamkasirisha yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
42 anHawakukumbuka uwezo wake,
siku aliyowakomboa kutoka kwa mtesi,
43 aosiku aliyoonyesha ishara zake za ajabu huko Misri,
maajabu yake huko Soani.
44 apAligeuza mito yao kuwa damu,
hawakuweza kunywa maji kutoka vijito vyao.
45 aqAliwapelekea makundi ya mainzi yakawala,
na vyura wakawaharibu.
46 arAliruhusu tunutu kuharibu mimea yao,
mazao yao kwa nzige.
47 asAliharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe
na mikuyu yao kwa mvua iliyochangamana na theluji.
48 atAliwaachia mifugo yao mvua ya mawe,
akayapiga makundi ya wanyama wao kwa radi.
49 auAliwafungulia hasira yake kali,
ghadhabu yake, hasira na uadui,
na kundi la malaika wa kuharibu.
50Aliitengenezea njia hasira yake,
hakuwaepusha na kifo,
bali aliwaachia tauni.
51 avAliwapiga wazaliwa wote wa kwanza wa Misri,
matunda ya kwanza ya ujana katika mahema ya Hamu.
52 awLakini aliwatoa watu wake kama kundi,
akawaongoza kama kondoo kupitia jangwani.
53 axAliwaongoza salama, wala hawakuogopa,
bali bahari iliwameza adui zao.
54 ayHivyo akawaleta hadi kwenye mpaka wa nchi yake takatifu,
hadi nchi ya vilima ambayo mkono wake wa kuume ulikuwa umeitwaa.
55 azAliyafukuza mataifa mbele yao,
na kuwagawia nchi zao kama urithi,
aliwakalisha makabila ya Israeli katika makao yao.

56Lakini wao walimjaribu Mungu,
na kuasi dhidi ya Yeye Aliye Juu Sana,
wala hawakuzishika sheria zake.
57 baKama baba zao, hawakuwa thabiti wala waaminifu,
wakawa wasioweza kutegemewa
kama upinde wenye kasoro.
58 bbWakamkasirisha Mungu kwa mahali pao pa juu pa kuabudia miungu,
wakachochea wivu wake kwa sanamu zao.
59 bcWakati Mungu alipowasikia, alikasirika sana,
akamkataa Israeli kabisa.
60 bdAkaiacha hema ya Shilo,
hema aliyokuwa ameiweka katikati ya wanadamu.
61 beAkalipeleka Sanduku la nguvu zake utumwani,
utukufu wake mikononi mwa adui.
62 bfAliachia watu wake wauawe kwa upanga,
akaukasirikia sana urithi wake.
63 bgMoto uliwaangamiza vijana wao,
na wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,
64 bhmakuhani wao waliuawa kwa upanga,
wala wajane wao hawakuweza kulia.

65 biNdipo Bwana alipoamka kama vile kuamka usingizini,
kama vile mtu aamkavyo kutoka kwenye bumbuazi la mvinyo.
66 bjAliwapiga na kuwashinda adui zake,
akawatia katika aibu ya milele.
67 bkNdipo alipozikataa hema za Yosefu,
hakulichagua kabila la Efraimu,
68 bllakini alilichagua kabila la Yuda,
Mlima Sayuni, ambao aliupenda.
69 bmAlijenga patakatifu pake kama vilele,
kama dunia ambayo aliimarisha milele.
70 bnAkamchagua Daudi mtumishi wake
na kumtoa kwenye mazizi ya kondoo.
71 boKutoka kuchunga kondoo alimleta
kuwa mchungaji wa watu wake Yakobo,
wa Israeli urithi wake.
72 bpNaye Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo,
kwa mikono ya ustadi aliwaongoza.
Copyright information for SwhNEN