‏ Haggai 1:2-15

2 aHivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Hawa watu husema, ‘Wakati haujawadia wa kujenga nyumba ya Bwana.’ ”

3 bKisha neno la Bwana likaja kupitia kwa nabii Hagai: 4 c“Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki, gofu?”

5 dSasa hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu. 6 eMmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.”

7Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu. 8 fPandeni milimani mkalete miti na kujenga nyumba, ili nipate kuifurahia, na nitukuzwe,” asema Bwana. 9 g“Mlitarajia mengi, kumbe, yametokea kidogo. Ulichokileta nyumbani nilikipeperusha. Kwa nini?” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Ni kwa sababu ya nyumba yangu, inayobaki katika hali ya magofu, wakati kila mmoja wenu anajishughulisha na nyumba yake mwenyewe. 10 hKwa hiyo, kwa sababu yenu mbingu zimezuia umande wake na ardhi mavuno yake. 11 iNiliita ukame mashambani na milimani, kwenye nafaka, mvinyo mpya, mafuta pamoja na chochote kinachozalishwa na ardhi, juu ya watu na ngʼombe, pamoja na kazi za mikono yenu.”

12 jKisha Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yoshua kuhani mkuu mwana wa Yehosadaki, pamoja na mabaki yote ya watu wakaitii sauti ya Bwana Mungu wao pamoja na ujumbe wa nabii Hagai, kwa sababu alikuwa ametumwa na Bwana Mungu wao. Watu walimwogopa Bwana.

13 kKisha Hagai, mjumbe wa Bwana, akawapa watu ujumbe huu wa Bwana: “Mimi niko pamoja nanyi,” asema Bwana. 14 lKwa hiyo Bwana akachochea roho ya Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na roho ya kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki, pamoja na roho za mabaki yote ya watu. Walikuja wakaanza kufanya kazi katika nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wao, 15 mkatika siku ya ishirini na nne mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario.

Copyright information for SwhNEN