‏ Proverbs 15

1 aJawabu la upole hugeuza ghadhabu,
bali neno liumizalo huchochea hasira.

2 bUlimi wa mwenye hekima husifu maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hufoka upumbavu.

3 cMacho ya Bwana yako kila mahali,
yakiwaangalia waovu na wema.

4 dUlimi uletao uponyaji ni mti wa uzima,
bali ulimi udanganyao huponda roho.

5Mpumbavu hubeza maonyo ya baba yake,
bali yeyote akubaliye maonyo huonyesha busara.

6 eNyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa,
bali mapato ya waovu huwaletea taabu.

7 fMidomo ya mwenye hekima hueneza maarifa,
bali sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu.

8 g Bwana huchukia sana dhabihu za waovu,
bali maombi ya wanyofu humfurahisha Mungu.

9 h Bwana huchukia sana njia ya waovu,
bali huwapenda wale wafuatao haki.

10 iAdhabu kali humngoja yeye aachaye njia;
yeye achukiaye maonyo atakufa.

11 jMauti
Yaani Sheol, maana yake ni Kuzimu.
na Uharibifu
Kwa Kiebrania ni Abadon.
viko wazi mbele za Bwana:
je, si zaidi sana mioyo ya wanadamu!

12Mwenye mzaha huchukia maonyo;
hatataka shauri kwa mwenye hekima.

13Moyo wenye furaha hufanya uso uchangamke,
bali maumivu ya moyoni huponda roho.

14Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hujilisha upumbavu.

15Siku zote za wanaoonewa ni za taabu,
bali moyo mchangamfu una karamu ya kudumu.

16 mAfadhali kuwa na kidogo pamoja na kumcha Bwana,
kuliko mali nyingi pamoja na ghasia.

17 nAfadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo
kuliko nyama ya ndama iliyonona pamoja na chuki.

18 oMtu mwepesi wa hasira huchochea ugomvi,
bali mtu mvumilivu hutuliza ugomvi.

19 pNjia ya mvivu imezibwa na miiba,
bali njia ya mwenye haki ni barabara kuu.

20 qMwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake,
bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.

21 rUpumbavu humfurahisha mtu ambaye hana akili,
bali mtu mwenye ufahamu hushika njia iliyonyooka.

22 sMipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri,
bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.

23 tMtu hupata furaha katika kutoa jibu linalofaa:
je, ni zuri namna gani neno lililotoka kwa wakati wake!

24 uMapito ya uzima huelekea juu kwa ajili ya wenye hekima
kumwepusha asiende chini kaburini.

25 v Bwana hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi,
bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe.

26 w Bwana huchukia sana mawazo ya mwovu,
bali mawazo ya wale walio safi humfurahisha yeye.

27 xMtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu,
bali yeye achukiaye rushwa ataishi.

28 yMoyo wa mwenye haki hupima majibu yake,
bali kinywa cha mwovu hufoka ubaya.

29 z Bwana yuko mbali na waovu,
bali husikia maombi ya wenye haki.

30 aaMtazamo wa tabasamu huleta furaha moyoni,
nazo habari njema huipa mifupa afya.

31 abYeye asikilizaye maonyo yatoayo uzima
atakuwa miongoni mwa wenye hekima.

32 acYeye anayedharau maonyo hujidharau mwenyewe,
bali yeyote anayekubali maonyo hupata ufahamu.

33 adKumcha Bwana humfundisha mtu hekima,
nao unyenyekevu huja kabla ya heshima.
Copyright information for SwhNEN