‏ Psalms 108

Kuomba Msaada Dhidi Ya Adui

(Zaburi 57:7-11; 60:5-12)

Wimbo. Zaburi ya Daudi.

1 aEe Mungu, moyo wangu ni thabiti;
nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
2 bAmka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
3Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa;
nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.
4 cKwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu;
uaminifu wako unazifikia anga.
5 dEe Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
utukufu wako na uenee duniani kote.

6 eTuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,
ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
7 fMungu amenena kutoka patakatifu pake:
“Nitaigawa Shekemu kwa ushindi
na kulipima Bonde la Sukothi.
8 gGileadi ni yangu, Manase ni yangu,
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,
nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
9 hMoabu ni sinia langu la kunawia,
juu ya Edomu natupa kiatu changu;
nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”

10 iNi nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome?
Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
11 jEe Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi,
na hutoki tena na majeshi yetu?
12 kTuletee msaada dhidi ya adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
13 lKwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,
naye atawaponda adui zetu.
Copyright information for SwhNEN